Header Ads Widget

Kisa cha Socrates


 

 KISA CHA SOCRATES NA MWANAFUNZI WAKE.


    Imeandikwa na Mwalimu Jumanne. 


Habari mfuatiliaji wa EKU FM?

 Ninayofuraha kwa kuwa wewe umeendelea kuwa msomaji wangu kwenye makala hizi za hamasa kwa ajili ya mafanikio makubwa. Usiache kupambana kwani yawezekana kesho jioni tu ndo siku Yako ya kutoboa. Wengi walikuwa na hali ya chini kuliko wewe lakini wameweza kupambana wakafanikiwa. Wengi walikuwa na elimu ndogo kuliko uliyonayo wewe lakini wamefanikiwa. Hakuna maisha mabaya bali kuna nyakati mbaya ambazo hazidumu.  Bado nipo mkoani Tabora nipo nyikani kujipika. Basi walau leo tupite na somo nilijifunza kutoka kwa mzee Socrates.


Socrates ni Muhenga wa kale sana kutoka Ugiriki ya kale. Tukisema Muhenga ni mzee mwenye akili nyingi japo siku hizi ukiitwa Muhenga na Binti ujue huna hili wala lile, yaani unakuwa umekosa hili dogo lakini mbaya zaidi hata lile nalo huna😂. Nimeongezea twende sawa. Socrates ni Moja wa wanafalsafa wa zamani sana ambao waliwahi kupita kwenye mgongo huu wa dunia na kuacha alama kubwa. Hii ndo faida ya kuishi na kuacha alama kubwa. Usikubali kufa ukiwa na hazina kubwa ndani Yako. Usiruhusu mimba ya wazi kubwa ulilobeba ukaitoa kabla ya kukomaa. Usife na wazo au ndoto. Kulitaja jina la marehemu humfanya aendelee kuishi tena. 



Ikumbukwe zamani kabla ya mapinduzi ya Viwanda elimu ilikuwa ikitolewa kwa mfumo wa Uanagenzi. Mwanagenzi ni mtu aliyebobea sana kwenye eneo fulani hivyo watu wanakwenda kujifunza. Kipindi hiki cha akina Socrates walikuwa wakikaa na wanafunzi wao kujifunza namna ya kufikiri mambo. Kufikiri ni kazi ngumu sana ndo maana wengi wanakimbilia kuhisi.  



Siku moja jioni, mwanafunzi mmoja wa Socrates alimuuliza mwalimu wake swali. "Mwalimu ipi siri kuu ya mafanikio?". Socrates akajibu je ni kweli unataka kuijua siri ya mafanikio? Mwanafunzi akajibu ndiyo ninataka kuijua. Socrates akamwambia kijana wake basi kesho Alfajiri uwahi sana tukutane ufukweni na huko nitakuambia siri kuu ya mafanikio. 



Mtaka cha uvunguni sharti ainame kijana aliwahi kuamka mapema mno kabla hakujapambazuka. Alitembea kwenye kigiza kuelekea huko ufukweni mwa bahari. Alipokaribia jirani tu aliweza kuona kivuli cha mtu lakini alipokikaribia alibaini alikuwa mwalimu wake tayari alikwisha kufika. Baada ya salamu fupi mwalimu alimwambia kijana wake atangulie wataingia baharini na huko ndiko atakwenda kumpa siri ya mafanikio. Kijana hakuwa anaelewa mwalimu wake alikuwa anakwenda kumpa siri gani ndani ya maji? Kwa kuwa yeye lengo lake ni kuipata siri hiyo alitii.


Ndani ya maji baridi, hatua za kutembea zikiendelea mwalimu nyuma mwanafunzi mbele. Hofu kwa mbali ndani ya kichwa cha mwanafunzi mrundikano wa maswali yasiyo na majibu. Maji yakazidi kuongezeka kina na kufika kifuani mwalimu akasisitiza twende. Mara maji shingoni kwa mwanafunzi, akazidi kujawa hofu ya kuzama ndani ya bahari.


Mara ikasikika sauti, SIMAMA!. Mwanafunzi akasimama lakini ghafla mwalimu akamkamata mabegani kwa nguvu na kumzamisha majini. Mwanafunzi akahamaki na kuanza kufurukuta ndani ya maji atoke lakini wapi. Mwalimu alizidi kumgandamiza tu kijana, alikuwa akipambana ajinasue kitu ambacho hakikuwezekana. Akiwa ameanza kuishiwa pumzi, na kumeza maji kiasi aliongeza pambano mpaka akachomoka mikononi mwa mwalimu wake akatoka. Alihema kwa nguvu kubwa na kuonekana kama amechanganyikwa. 


Mwalimu akaanza kurudi kwenye ufukwe wa bahari bila kuongea neno. Mwanafunzi alizidi kumrushia maswali mwalimu tena kwa kufoka. Kwanini unataka kuniua? Alisahau hata swali lake la Msingi ambalo ni Nini haswa siri kuu ya mafanikio? Mwalimu akamjibu kwa kuuliza swali? Kwani ulipokuwa  ndani ya maji kitu gani hasa ulikosa? Akasema kijana pumzi nilishindwa kuvuta hewa ya Oksijeni. Nilikuwa naelekea kufa kwa kushindwa kupumua. 


Basi kijana wangu siri ya mafanikio kama ulivyokuwa unapambana kuipata hewa ya Oksijeni hivyo ndivyo unatakiwa uyapambanie mafanikio yako.  Chochote unachotaka maishani kipambanie kama ulivyokuwa ukiitaka hewa baada ya kuipoteza. Kwa heri nenda kafanikiwe mara dufu. Baada ya ubatizo huo mwalimu akaenda zake.


Funzo.


🌚Oksijeni ni kile kitu cha Msingi unakihitaji. Nini umekosa hapo ulipo? Fedha? Ajira? Mtaji? Connection? Ndoa? Watoto hawakuelewi?  Basi fahamu kuwa kitakacho kupa hicho ni hiki👇🏿


🌚Shauku, ni ile hali ya kuingiwa na roho ya Uungu ndani yako. Kupata hamasa kubwa ndani yako kulifanya jambo lisilo la kawaida. Kupata kiu kubwa ya kupata chochote Unachotaka. Kama ni ajira utaipata au fedha utazipata. Kama hujapata ujue bado shauku yako ni ya chini sana. Kila unachokifanya kifanye kwa dhati, kifanye kwa viwango vikubwa na kwa ufanisi. Jitoe kukifanya bila kujali hatari wala kumuogopa mtu. Kipambanie kana kwamba ndiyo kitu cha mwisho kwako kukifanya hapa duniani. Fanya kitu hiko kwa mara ya kwanza na kwa mara ya mwisho. Kuhusu maumivu makali hayakwepeki.


🌚 Bahati ni maandalizi yalokutana na fursa. Bado unaamini kwenye bahati? Ni ukweli usiopingika kuwa  wapo watu wanapata bahati nasibu maishani mwao, wanabet na kupata hela nyingi. Wapo wanaorithishwa mali nyingi kutoka kwa marehemu wao. Lakini wewe haitatokea  upate hivyo. Yaani haiwezekani utajirike kirahisi wewe. Wewe andika maneno haya "HAKUNA NJIA YA MKATO KWENYE KUTAFUTA MAFANIKIO, NJIA HIYO HAIJAWAHI KUWEPO, HAIPO NA HAITAKUJA KUWEPO"Kitakacho kutajirisha ni kuamka Sasa hivi kwenda ukajitoe kafara ya  jasho, damu na machozi. Kama kichwa chako hakijakatwa basi una nafasi kubwa ya kufanikiwa.  Usilale mchana wakati ndoto hazijatimia.


Kama umekosa Oksijeni pambana uipate ukizubaa unakufa kwenye maji. Kila siku moja ya maisha yako unayojisahau kuchukua hatua fulani ya maisha yako unapoteza kipande kikubwa cha thamani ya maisha yako.Kila maamuzi unayoshindwa kuyachukua leo kwasababu ya visingizio vya aina yoyote vilivyopo kuna sehemu ya maisha yako inayopotea bila taarifa.Usipoanza kufanya kitu leo kwa chochote na uwezo ulionao leo .unapoteza Fursa nyingine ambayo ungekutana nayo kesho kama ukifanya maamuzi yako leo.Maisha si sanaa ya kuamka asubuhi kutafuta pesa ya kulipa kodi ya nyumba na bili nyingine zote. Maisha ni zaidi ya hayo yote. Hatukuja duniani kuja kulipia bili. 


🌚Kwa kuhitimisha leo, naomba niendelee kukukaribisha kwenye mchakato wa kuweka akiba na kufanya Uwekezaji. Ni mchakato wa taratibu wa kuweka fedha kidogo kidogo ili kuuelekea uhuru wa kiuchumi. Kumbuka kuweka akiba ni mbegu ya utajiri. 


Basi ukawe na wakati mwema, 

USIKUBALI MAONO MAKUBWA ULIYONAYO YAFE KIRAHISI. KUFA HAUJAFANIKIWA NI UBINAFSI NA ROHO MBAYA. USIRUDI NA ZAWADI ULIPEWA UIKABIDHI DUNIA. ENDELEA KUFUATILIA NAKALA ZOTE HAPA EKU FM.

Post a Comment

0 Comments